Alhamisi 3 Septemba 2026 - 11:30
Imam Musa Sadr Alikuwa Mlinganiaji wa Haki na Umoja; Sisi Bado Tupo Juu ya Ahadi Ile Ile

Hawzah/ Sheikh Hassan al-Baghdadi, mjumbe wa Baraza Kuu la Hizbullah, amesema katika maadhimisho ya kutekwa kwa Imam Musa Sadr na wenzake kwamba katika kumbukumbu hii, ni lazima tufanye upya kiapo chetu cha utii kwa Imam Musa Sadr na kusisitiza kushikamana kwetu na njia aliyoianzisha.

Kwa mujibu wa Idara ya Tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, katika kumbukumbu ya miaka 48 ya uhalifu wa kutekwa Imam wa Muqawama, Sayyid Musa Sadr, pamoja na masahaba wake wawili, Sheikh Muhammad Yaqub na mwandishi wa habari Abbas Badruddin, Hujjatul-Islam Sheikh Hassan al-Baghdadi, mjumbe wa Baraza Kuu la Hizbullah, amesema:

Katika kumbukumbu hii, tunapaswa kufanya upya kiapo chetu cha utii kwa Imam Musa Sadr na kusisitiza kushikamana kwetu na njia aliyoianzisha; njia ya Muqawama dhidi ya ukaliaji wa mabavu, kukabiliana na ufisadi na kupambana dhidi ya kunyimwa haki. Vichwa hivi, licha ya kuwa ni vingi, vinakusanyika katika kichwa kimoja: haki; haki ile ambayo imepotea miongoni mwa viongozi na sehemu kubwa ya nguvu na watu wanaosimamia mambo ya umma.

Sheikh al-Baghdadi aliongeza: Matumaini bado yapo, licha ya maumivu ambayo hayawezi kuelezwa na pengo lisiloweza kuzibwa, yaani kumpoteza kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Shahidi Sayyid Ali Khamenei (Mwenyezi Mungu autukuze utakatifu wa roho yake), pamoja na shahidi wa Umma, Sayyid Hassan Nasrullah (Mwenyezi Mungu amridhie), na pamoja nao makamanda wakuu na mashujaa.

Lakini kinachotupa faraja ni kwamba sisi ni Umma ambao tumezoea kuwapoteza viongozi na kutoa mashahidi. Na ndani ya Umma huu kuna kheri nyingi, pamoja na makamanda wenye uwezo wa kubeba majukumu; watu ambao wamepitia vita vikali zaidi na wakapata ushindi ndani yake.

Aliendelea kusema: Ninachotaka kusema katika kumbukumbu hii, ewe Sayyid mtukufu, ni kwamba bado tupo juu ya ahadi ile uliotuachia. Bado tunashikamana na chaguo la Muqawama, kukabiliana na ufisadi wa madaraka na kupambana dhidi ya kunyimwa haki, kila mmoja kwa kadiri ya uwezo wake.

Vilevile, tumejitolea kushikamana na chaguo la umoja wa Waislamu, kuleta ukaribu baina ya madhehebu ya Kiislamu na umoja wa kitaifa.

Alibainisha kwamba: Ewe Sayyid mwenye heshima kubwa, ulikuwa ukiwaita watu wote wenye ikhlasi kushikamana na umoja wa Waislamu, na ulikuwa ukipendekeza mambo yenye kuunganisha Umma; kuanzia kuifanya siku ya Eid kuwa moja na kusimama Arafa siku moja, hadi kushikamana na suala la Palestina kama jambo linalouunganisha Umma wote.

Mjumbe huyo mwandamizi wa Hizbullah alisisitiza: Umma unapaswa kusimama kwa ajili ya kuikomboa Palestina, kwa sababu hili si suala la Wapalestina pekee, wala si suala la madhehebu au kundi fulani, bali ni suala la Umma kwa matabaka yake yote.

Palestina, katika mradi wa Kizayuni, si ardhi inayokaliwa kwa mabavu pekee, bali ni ngome na njia ya kupitisha mradi mpana zaidi unaotishia ulimwengu mzima wa Kiarabu, ndani ya mfumo wa kile kinachoitwa “Israel Kubwa.”

Hili ndilo lililoonekana wazi zaidi baada ya operesheni ya Tufani ya Al-Aqsa; operesheni ambayo wavamizi waliifanya kuwa kisingizio cha kuanza kutekeleza mradi huu wa upanuzi.

Sheikh al-Baghdadi pia alimwambia Imam Musa Sadr: Wewe, wakati huohuo, ulikuwa ukisisitiza uzuri wa utofauti na wingi wa kimadhehebu nchini Lebanon, na uliamini kwamba tatizo haliko katika kuwepo madhehebu na dini mbalimbali, bali liko kwa viongozi wafisadi ambao hugeuza tofauti hizi kuwa chombo cha kugawanya watu na kuwanyonya.

Kwa hiyo, katika kumbukumbu hii, tunafanya upya kiapo chetu cha utii na kusisitiza kwamba hatutaachana na misingi hii, na tutashikamana na misingi hii na misimamo hii, hata kama tutatoa mashahidi wengi kiasi gani na hata kama majeraha yetu yatazidi kuwa ya kina kwa kiasi gani.

Sheikh al-Baghdadi alimalizia kwa kusema: Tutasubiri, tutamwachia Mwenyezi Mungu malipo yetu na tutaendelea na njia hii, tukiwa na yakini kwamba Mwenyezi Mungu hatapoteza malipo ya wenye kusubiri na atatupa ushindi dhidi ya maadui zetu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha